MWANDISHI FEKI ANASWA




Stori:Haruni Sanchawa
Kampuni ya Global Publishers & General Enterprises Ltd, inayochapisha Magazeti Pendwa ya Uwazi, Ijumaa, Risasi, Amani, Ijumaa Wikienda na Championi, siku zote ipo mstari wa mbele kupinga vitendo vya rushwa.

Global, ikitambulika hivyo kijamii, kijana anayeitwa Mpemba Masala alithubutu kufanya utapeli akijitambulisha kuwa ni Mwandishi wa Gazeti la Ijumaa lakini akakamatwa kabla ya kufanikisha uhuni wake.
Mpemba ambaye hutumia pia jina la Hilary Msili katika matukio yake ya utapeli, anadaiwa kushirikiana na wenzake kumtishia mwanamke ambaye ni daktari mkazi wa Tegeta, Kinondoni, Dar es Salaam ili kujipatia fedha.

Inadaiwa kwamba Mpemba akiwa na wenzake, walimtishia daktari huyo mwanamke kuwa wao ni waandishi wa habari kutoka Gazeti la Ijumaa, kwamba wana picha zake za utupu, wakamtaka awape shilingi 500,000, vinginevyo wangemtoa gazetini.
ALIVYONASWA
Timu ya Global Publishers ikiwa katika utekelezaji wake wa majukumu ya kila siku, Jumapili iliyopita, ilipokea taarifa za kuwepo kwa kikundi hicho cha watu kinachoipaka matope kampuni hiyo, iliyojipatia heshima kwenye jamii kutokana na kazi yake ya kufichua maovu.
Baada ya kupokea taarifa hizo, Global ilitengeneza kikosi kazi ambacho kiliingia kazini mara moja, shabaha kuu ikiwa kukinasa kikudi hicho cha matapeli na kukifikisha kwenye mikono ya sheria.
Kikosi kazi kutoka Global, kiliunganisha nguvu na askari wa Kituo cha Polisi Kawe, kwa kumtumia mwanamke huyo, kilimtega mtuhumiwa huyo wa utapeli na kufanikiwa kumnasa siku hiyohiyo (Jumapili).
Hata hivyo, Mpemba alikamatwa peke yake kwani ndiye aliyetumwa na wenzake kuwawakilisha katika kupokea fedha kutoka kwa mwanamke huyo.

ILIVYOKUWA
Kwa kawaida Global hufanya kazi zake kisayansi, kwa hiyo baada ya kuingia kazini ilihakikisha mwanamke huyo anatuma SMS kwenda kwa kikundi hicho, iliyosomeka:
“Fedha, shilingi 500,000 mlizohitaji zipo tayari, tukutane niwape.”
Haraka sana, SMS hiyo ilijibiwa na matapeli hao, wakitaka kujua sehemu ya kukutana.
Baada ya kuambiwa sehemu hiyo, Mpemba alitokea peke yake na wakati akijiandaa kupokea fedha hizo kutoka kwa daktari huyo wa kike, alijikuta anawekwa nguvuni na polisi huku kikosi kazi cha Global kikiwa ‘bize’ na uchukuaji wa picha.

TAPELI KIBOKO
Baada ya Mpemba kukamatwa, alikutwa na simu zenye namba mbili, kila moja ikiwa imesajiliwa kwa jina lake.
Simu ya kwanza ni mtandao wa Airtel, nambari 0683686600, imesajiliwa kwa jina Mpemba Masala, nyingine ni Tigo, 0717547325, jina la usajili ni Hilary Msili.
Kutokana na mazingira hayo, Polisi Kawe walimfungulia mashitaka katika kitabu cha kumbukumbu za polisi (Report Book ‘RB’), nambari KW/RB/6550/2013 KUJIFANYA MWANDISHI WA HABARI.

AMTAJA BOSI WAKE
Mpemba baada ya kubanwa, aliweza kumtaja mkuu wa kikundi chao cha utapeli kwamba anaitwa Greyson J Kashinje ambaye ni mtaaluma wa IT.

TAMKO KUTOKA GLOBAL
Mhariri Kiongozi wa Magazeti pendwa, Global Publishers Ltd alisema kuwa watu wanatakiwa kuwa makini na utapeli unaofanywa na watu wanaojitambulisha kwamba ni waandishi wa habari wa kampuni hiyo.
“Watu wanaibiwa sana kwa udanganyifu huo, wanapigiwa simu na watu wanaojifanya ni waandishi wa habari, wanadai wana habari zao mbaya kwa hiyo wanahitaji wakutane wamalizane.
“Kwanza itambulike kuwa anayefanya hivyo siyo mwandishi wa habari. Mwandishi mwenye weledi anajua maadili yanasemaje. Hao ni matapeli, jamii iwe makini nao,” alisema na kuongeza:
“Kwetu Global hakuna rushwa, tupo makini na tunazingatia sana maadili. Kama mtu yeyote anatishwa na mtu anayejitambulisha kuwa ni mwandishi wa habari kutoka Global Publishers, apige simu nambari 0754290167, tutamsaidia kuwakamata matapeli hao.”

0 comments:

Post a Comment