ZITTO, MBATIA NA MAKAMBA WATAJWA KWA URAIS 2015


Pia wamo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na Dk Hussein Mwinyi na  wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo.
Dar es Salaam. Ikiwa imebaki miaka miwili kufanyika ka uchaguzi mkuu nchini, Kamati ya Vijana wapenda Amani Tanzania, imetaja majina ya watu wanne wenye sifa za kuwania urais nchini, huku ikieleza kuwa uzoefu wa miaka mingi si kipimo kizuri cha uongozi bora.
Kamati hiyo imesema Watanzania wanatakiwa kuwaogopa watu wanaojitaja wazi kuutaka urais, huku wakitumia majukwaa ya kisiasa, kidini, kijamii, kiutamaduni na michezo kutoa misaada mbalimbali kwa maelezo kuwa watu hao wakipewa nchi, wataongoza kwa maslahi ya kundi fulani.
Waliotajwa katika orodha hiyo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi na Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Katika orodha hiyo, kamati hiyo haikuwataja viongozi waliowahi kujitangaza kutaka nafasi hiyo na ambao hawajajitangaza, lakini wanaonekana kuwa na dhamira ya kugombea urais mwaka 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Chifu Msopa, alisema wakati umefika kujadili mahitaji ya nchi kiuongozi kwa manufaa ya siku zijazo,.
Katika maelezo yake, Msopa alitaja sifa za kila kiongozi aliyemtaja katika orodha hiyo na kwamba  kama ikitokea watu hao wakashindwa kusimamishwa na vyama vyao kuwania urais mwaka 2015,  kamati hiyo itamuunga mkono  yeyote ambaye atakuwa na sifa zinazofanana na watu hao wanne.
Sifa za waliotajwa
Kwa upande wa ZittoMsopa alisema ana uwezo mkubwa kiungozi, na kwamba mfano ni wa jinsi anavyosimamia Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na kufichua madudu.
Kwa upande wa Mbatia, alisema kiongozi huyo ni mzalendo wa nchi yake, ametulia na ana hekima kubwa ya kiuongozi na kwamba busara zake zimedhihirika kwa jinsi anavyoongoza Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kama mwenyekiti.
“Amekuwa akipigania ubora wa elimu ya watoto wetu na kujali ujenzi wa taifa bora zaidi na ana uwezo wa kufanya kazi na viongozi kutoka vyama vyote vya siasa.
Akitaja sifa za Makamba alisema wakati akiwa mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini alikuwa msema kweli, jasiri kwa kuikosoa Serikali inayoongozwa na chama chake.
Alisema Makamba wakati akiwa Wizara ya Mambo ya Nje, alikuwa msaidizi wa Rais Jakaya Kikwete kwa miaka mitano na kufafanua kuwa hiyo ni sifa ya muhimu kwa kiongozi.
Akimzungumzia Dk Mwinyi, Msopa alisema ana busara na ndio sababu ya kuongoza vizuri wizara nyeti ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

0 comments:

Post a Comment