NI VITA,MASAA 48 YANAKARIBIA KUISHA,WAASI WA M23 WAAMBIWA WAJISALIMIESHE..VINGINEVYO NI HATARI


U   Wanajeshi wa Brigedi Maalum wakiwa katika mazoezi makali yaliyofanyika hivi karibuni huko Goma Mashariki ya Demokrasia ya congo

 Mmoja wa walinda amani kupitia Brigedi Maalum inayoundwa na wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi akiwa katika moja ya mazoezi yaliyofanyika hivi karibu huko Goma.
 Kamanda Mkuu wa Misheni ya Kulinda Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ( MONUSCO ) Luteni Jenerali Carlos Albeto dos Santos Cruz ametakanza jana jumanne akiwa Goma kwamba MONUSCO itaanza rasmi kuitumia Brigedi Maalum na ametoa saa 48 kuanzia saa kumi jioni kwa saa za Goma jana siku ya Jumanne waasi wote kusalimisha silaha zao, na kwamba ifikapo saa kumi jioni kwa saa za Goma siku ya Alhamisi Agosti Mosi wale wote ambao watakuwa hawajasalimisha silaha zao watachukuliwa kama tishio la usalama kwa wananchi na MONUSCO italazimika kuwapokonya ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu kwa mujibu wa Mamlaka iliyopewa na Sheria zinazowaruhusu kufanya hivyo.
------------------------------

Misheni ya Kutuliza   Amani katika  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  ( MONUSCO) imetangaza  kwamba kwa mara ya kwanza itaanza kuitumia Brigedi Maalum ( Force Intervention  Brigade)  katika kudhibiti  eneo  maalum  la usalama  ( security zone ) kuzunguka  mji wa Goma ulioko   Mashariki ya  Jamhuri ya  Kidemokrasia ya Kongo na imewapa  saa 48 waasi kusalimisha silaha zao.

Taarifa iliyotolewa na  MONUSCO na kusambazwa na   Idara ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa  jana  jumanne,  inaeleza kwamba watu binafsi katika eneo la   Kivu ya Magharibi ambalo linajumisha Goma na  Sake  na ambao hawahusiki na vyombo vya usalama watapewa saa 48 kuanzia saa kumi jana kwa saa za Goma ( Jumanne ) kuzisalimisha silaha zao katika  Misheni hiyo na  kujiunga na mchakato wa DDR/RR unaoratibu upokonyaji, usambaratishaji,  urejeshwaji makwao, kuwaunganisha  na jamii na kuwapatia makazi.  

Baada ya  saa  kumi jioni ya  Alhamisi, Agosti Mosi. Taarifa hiyo inasema. Wale wote ambao watakuwa hawajasalimisha silaha zao watachukuliwa kama  tishio kwa usalama wa  wananchi na MONUSCO itachukua hatua zote muhimu kuwapokonya silaha hizo ikiwa ni pamoja  na kutumia nguvu kama ilivyoainishwa katika Mamlaka na sheria za  ushiriki  za  MONOSCO. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo zaidi ya wananchi milioni moja wanaishi katika eneo dogo la Goma na Sake na kando kando ya barabara  ambayo inawaunganisha na   kambi ya wakimbizi ya Mugungu ambayo ni  makazi ya  muda ya watu  karibu 70, 000 ambao wameyakimbia makazi yao kutokana na mapigano.

Kwa mujibu wa MONUSCO, tangu kati kati ya mwezi Mei eneo hilo limeshuhudia mapigano ya mara kwa mara kutoka kwa kundi la M23 dhidi ya  majeshi ya Serikali  ya  FARDC ikiwa ni  jaribio la   wazi la kutaka  kusonga mbele kuelekea Goma na Sake.

“ Katika mashambulizi hayo, likiwamo la hivi karibuni la Julai 14, M23 walitumia  kiholela silaha zao  za  moto zikiwamo silaha nzito  ambazo zimesababisha  wananchi kujeruhiwa” .
Taarifa hiyo imeongeza kwamba    kundi hilo la M23 katika mashambulizi hayo  limelenga pia Vituo vya Umoja wa Mataifa.
Aidha  taarifa hiyo inabainisha kwamba  eneo hilo maalum la usalama ( security zone)  litasaidia kudhibiti tishio la moja kwa moja  mbali na eneo la  nje ya Goma na pengine  eneo hilo linaweza kupanuliwa na kurudiwa sehemu  nyingine  kutakako hitajika.
 Tamko hilo  la kutoa saa 48 kwa waasi kusalimisha silaha zao  linafuatia kuwasili  katika eneo la Goma kwa  Kamanda Mkuu wa  MONUSCO, Luteni    Jenerali  Carlos Alberto dos Santos Cruz, ambaye alitangaza kwamba  Misheni ya MONUSCO itaunga mkono jeshi la Serikali  ( FARDC)  katika kuanzisha eneo la usalama kuzunguma  eneo la  Goma na vitongoji vyake.
 
Taarifa hiyo inamkariri Kamanda  Mkuu wa MONUSCO akiyapongeza  majeshi ya serikali  kwa  kazi nzuri iliyofanya wiki  iliyopita ya kuwadhibiti M23. Ingawa  anasema eneo la Goma na Sake   bado limo katika mazingira magumu sana na kwamba ni wajibu wa wahusika wote kuhakikisha wahalifu wote hawaendelei kuhatarisha  raia wa eneo hilo.
Kwa mwaka uliopitia , kundi la M23 pamoja na makundi mengine yenye silaha yamekuwa yakipambana mara kwa mara na majeshi ya serikali katika  Mashariki ya Kongo, huku  makundi hayo yenye silaha  mwezi Novemba mwaka jana yakiikalia Goma  kwa muda.
Aidha mapingano ya hivi karibuni  ambayo safari hii yalihusisha pia kundi jingine la wanagambo wenye silaha  lenye asili yake nchini Uganda, yamesababisha zaidi ya wananchi 100,000  kuyakimbia makazi yao na hivyo kuongeza mgogoro  wa kibinadamu katika eneo hilo linalohusisha watu wengine 2.6 milioni ambao wameyakimbia makazi yao huku wengine 6.4 milioni wakihitaji  chakula na  huduma za dharura.
Wakati huo huo,   Kaimu Mkuu wa  MONUSCO  Bw. Moustapha Soumare  katika taarifa  yake ametoa wito kwa pande zote kutafuta suluhu ya kisiasa  kwa   matatizo ya  DRC kupitia Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa kuhusu amani, usalama  na  ushirikiano wa maendeleo katika DRC na  eneo la Maziwa  Makuu uliopitisha mwezi wa Februari na viongozi 11 wa Afrika na  Taasisi nne za  Kikanda na Kimataifa.

Aidha akasema  katika  kipindi hiki ambacho suluhu la kisiasa linatafutwa MONUSCO itatumia nguvu iliyonayo kuwalinda wananchi dhidi ya hatari zitokanazo na  makundi ya waasi

0 comments:

Post a Comment