Watumia gari kutapeli Sh 470,000/=


POLISI mkoani Dodoma inashikilia watu watatu wakiwemo raia wa nje, kwa tuhuma za kufanya utapeli na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika vituo vya kuuzia mafuta na maduka ya kubadilishia fedha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema tukio hilo ni la jana katika Kituo cha Camel kilichoko Chuo cha Mipango katika Manispaa ya Dodoma. Misime alisema watu hao walifika katika kituo hicho ambapo kulikuwa na duka na kuagiza soda kisha baadaye kutoa dola 50 ya Marekani.
Inadaiwa muuzaji aliwaambia watu hao kwamba habadilishi fedha, hivyo kuamua kumdanganya kuwa wanahitaji fedha ya Kitanzania kwa ajili ya kwenda kuonesha Misri kama sehemu ya maonesho.
“Wateja hao waliomba wapatiwe noti za 10,000 za zamani ili wao wampatie noti mpya za 10,000 , muuzaji huyo alichambua noti za zamani zipatazo Sh 470,000 na kuwapa kisha wao kumwambia wanazotaka kumbadilishia ziko kwenye gari na kujifanya kwenda katika gari na matokeo yake waliondoka kwa kasi,” alisema Kamanda.
Alisema baada ya watu hao kuondoka kwa kasi, ndipo muuzaji huyo aligundua kwamba ameibiwa na kupiga simu Polisi ambao waliwasiliana na vituo vyote vya mjini na nje ya mji na kufanikiwa kuwakamata matapeli hao katika kituo cha Chanene kilichoko wilayani Chamwino Pori la Mtungutu.
Kwa mujibu wa Kamanda, watu hao walikuwa wakitumia gari aina RAV 4 T. 872 CGE lenye rangi ya damu ya mzee.
Aliwataja watu hao wenye asili ya Kiarabu ni mwanamke Ahlam Hassan, (50) mkazi wa Tanga, raia wa Sudan aliyekuwa dereva Daoud Abdelgawad (39).
Abdelgawad ambaye ni mkazi wa Misri, inadaiwa alikuwa na hati ya kusafiria ikionesha aliingia nchini Julai 19 mwaka huu na viza ya kuishi nchini kwa miezi mitatu.
Wengine wanaotuhumiwa kufanya utapeli huo ni Matata Lawrence (38) ambaye ni dereva na Mkazi wa Gongo la Mboto, Rahma Mahamoud (26) Mkazi wa Dar es Salaam pamoja na Salehe Mnene (40) ambaye ni mkazi wa Manzese, Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi amehadharisha wananchi kuwa makini na matapeli.
Aidha ametaka kutoa taarifa haraka polisi juu ya watu wanaowatilia shaka ili hatua za kuwadhibiti zichukuliwe mapema.
chanzo-habari leo

0 comments:

Post a Comment