VIONGOZI wa Chama cha Msingi cha
Ushirika wa Mazao na Masoko Lenganelo na Diwani wa Mchemo, Mshamu
Chituta, wamekamatwa na wanachama, wakafungiwa katika ghala la korosho
na kumwagiwa upupu.
Akizungumzia kisa hicho katika Baraza la
Madiwani juzi, diwani huyo alisema wanachama hao walishikwa na hasira
mkutanoni, baada ya kudanganywa, ndipo walipomkamata yeye na uongozi wa
chama hicho na kuwafungia kisha kuwamwagia upupu.
Alitaja wenzake waliopata adhabu hiyo
kuwa ni Mwenyekiti wa Chama hicho, Hassan Nakuya, Katibu aliyemkumbuka
kwa jina moja la Mnali na msaidizi wake, Ramadhani Mpanga. Chituta
alisema uongozi wa chama hicho, ulitangazia wananchi kwenye mkutano huo,
kuwa Mkuu wa Wilaya ya Newala, Christopher Magalla, angekuwapo.
Habari kutoka eneo la tukio, zilieleza
kuwa viongozi wa chama hicho walitumia jina la Mkuu wa Wilaya kuitisha
mkutano wa wanachama, ili kuwavuta wahudhurie kwa wingi. Diwani Mshamu
alisema hakuwa anajua kama uongo ulitumika, kwa kuwa siku ya tukio
alikuwa na kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, lakini aliombwa na
Katibu wa Chama cha msingi, asitishe kikao hicho na aende kwenye mkutano
wa chama ambao pia ungehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya.
Kwa mujibu wa diwani huyo, wanachama
waliitika mwito lakini mkutano ulianza bila Mkuu wa Wilaya, wakagundua
kudanganywa ndipo wakaamua kuwaadhibu viongozi na yeye kwa kuwafungia
ghalani na kuwamwagia upupu.
Alisema walijaribu kuwasiliana na Mkuu
wa Wilaya, ili afike kuwanusuru, lakini simu yake haikupatikana hivyo
wakakaa ghalani kwa saa kadhaa, mpaka walipomtafuta Mkuu wa Polisi wa
Wilaya (OCD), aliyefika kuwafungulia.
Kutokana na malalamiko hayo ya diwani
katika Baraza hilo ambalo Magalla pia alihudhuria, Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Newala, Ashidi Ndembo, alimwomba Mkuu wa Wilaya, kutoa
ufafanuzi wa suala hilo, ili kuondoa hali ya sintofahamu baina ya diwani
na uongozi wa chama cha msingi. Majibu ya DC Akijibu hoja hizo, Magalla
alisema hakuwa na taarifa na mkutano huo na kwamba siku inayotajwa
kufanyika mkutano huo, alikuwa kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na
Usalama cha Mkoa mjini Mtwara.
“Nataka nichukue nafasi hii kueleza
kwamba sikuwa na taarifa ya mkutano huo, siku hiyo nilikuwa katika kikao
mjini Mtwara na simu nilizima kutwa nzima. Nilipoiwasha, nilikuta
ujumbe kutoka kwa mtu nisiyemjua, nilipopiga simu nikagundua ni
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Lenganelo,” alisema Magalla.
Alisema baada ya kumpigia, Mwenyekiti
huyo alimfahamisha kuwa alikuwa amefungiwa ghalani na wakulima na
alimpigia kutaka msaada lakini simu haikupokewa, ingawa
walishafunguliwa. Magalla alionya wanaotumia jina lake kuitisha mikutano
ya wananchi kwa kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria na utovu wa
nidhamu, alitaka wahusika wa jambo hilo waache kabla hatua za kisheria
hazijachukuliwa dhidi yao.
“Nimesikitishwa sana na kitendo hiki,
hasa ninaposikia kinafanywa na viongozi wenzangu. Kwa kweli si jambo
jema…tunajua kuna baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa hawajitokezi
wanapoitwa katika vikao na mikutano, sasa kama viongozi wa eneo hilo
wanahitaji msaada wa DC, ni vema wakawasiliana nami na kwa kuwa huo ni
wajibu wangu nitakuja,” alisema Magalla.
chanzo-habari leo
0 comments:
Post a Comment