'Hekalu' linalomilikiwa na Mchungaji Getrude Lwakatare.
|
|
|
Wabunge wamemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira Terezya Huvisa kuzivunja nyumba mbili zilizopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam zilizojengwa katika..
Bila kutaja majina ya wamiliki hao, wabunge hao walitaka hatua hizo zichukuliwe kwa haraka kwa nyumba hizo zilizojengwa kwenye fukwe kinyume cha sheria zivunjwe kwa maelezo kuwa hazina ofa wala hati.
Sambamba na hilo wametaka watendaji wa serikali waliohusika kutoa vibali kuruhusu ujenzi huo kwa maelezo kuwa walichukua rushwa wachukuliwe hatua.
Mbunge wa kwanza kuanza kuzungumzia hilo ni wa viti maalum, Esther Bulaya (CCM) aliyetaja viwanja viwili vyenye namba 2019 na 2020 kikiwemo cha mbunge ambaye ni kiongozi wa kiimani waliojenga nyumba zivunjwe licha ya kuwepo zuio la mahakama.
“Mwaka jana waziri wa Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka alivunja nyumba za kawaida licha ya zuio la mahakama, lakini nyumba zilizo kwenye viwanja namba 2019 na 2020 hazikuvunjwa kwa sababu ya zuio la mahakama hii ni double standard hatuwezi kuvumilia.
“Wengine wenye nyumba ni viongozi tupo nao humu tena wa kiimani, lakini kwa nini viongozi tunafaya hivi wakati tunatakiwa tuwe wa mfano na tunawafanya viongozi wenzetu washindwe kufanya kazi zao?…hakuna haja ya kuogopa waziri Huvisa (Mazingira) vunja nyumba, haiwezekani kuwa na nguvu ya fedha.
“Wabunge wenzangu tuazimie Manispaa ya Kinondoni na NEMC (Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira), wakavunje nyumba hizo ndani ya wiki moja , naomba kutoa hoja,” alisema.
Hata hivyo, Spika Anne Makinda alimweleza; “Haiwezekani kutoa hoja kwa kuingilia vyombo vingine”.
Mbunge ambaye ni kiongozi wa kiimani mwenye nyumba katika eneo hilo la Mbezi Beach aliyejenga katika fukwe ya bahari kwa kuondoa mikoko na kuweka kifusi na kujenga nyumba ni Mbunge wa Viti Maalumu, Mchungaji Dk. Getrude Lwakatare (CCM).
Naye Mbunge wa viti maalumu, Grace Kiwelu (Chadema) akichangia bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, alisema kamati yake ya Ardhi na Mazingira ilitembelea eneo hilo la Mbezi Beach na kukuta aliyejenga katika kiwanja 2019 hakuwa na ofa wala hati.
“Ametumia pesa kuwarubuni watendaji akaondoa mikoko, akaweka kifusi na akajenga nyumba naomba wizara ya Ardhi na ya mazingira wawachukulie hatua watendaiji hao,” alisema.
Akijibu hoja ya Bulaya, kuwa kwanini nyumba ya Mchungaji Lwakatare haikuvunjwa wakati nyingine zilivunjwa, mwanasheria mkuu wa Serikali, Frederick Werema alisema:
“Sisi ni wajibu wetu twende mahakamani kusema watu hao wamevunja sheria kujenga hapo. Wao wanaruhusiwa na Katiba na mahakama itafuata sheria.
“Nashauri Bulaya usitoe shilingi kuzuia Bajeti ya Waziri, uje tuone huyo kigogo itakuwaje.”
Hata hivyo, Huvisa alisema: “Nyumba tulizovunja hazikuwa na kesi na hii tuliyoiacha ilikuwa na kesi.”
Jumba la kifahari linalodaiwa kuwa la Mchungaji Lwakatare ambalo lilizinduliwa mwaka jana, limekuwa klikitajwa kuwa lina thamani ya takribani sh bilioni 1.5.
zero99