FFU WAPINDUKA, MMOJA AFARIKI, WAKIENDA KUTEMBEZA KICHAPO



ASKARI mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoani Kilimanjaro, Fidelis Mwaliyatabu, amefariki dunia papo hapo na wengine tisa akiwamo Mkuu wa Kikosi hicho kujeruhiwa vibaya baada ya gari lao kupinduka katika kijiji cha Kilingi, wilaya ya Siha, wakati wakienda kuzima vurugu za wananchi.
Ajali hiyo ilitokea wakati kikosi hicho kikielekea katika kijiji cha Karansi kwa ajili ya kukabiliana na wananchi waliokuwa wakiandamana kupinga wenzao waliokamatwa usiku wa manane baada ya kuvamia mashamba mali ya Shirika la Roho Mtakatifu-Kilasara.
Taarifa kutoka kijijini humo zilieleza kwamba wanakijiji waliamua kuandamana baada ya wenzao watano kukamatwa na Jeshi la Polisi nyakati za usiku kwa mahojiano kutokana na kukabiliwa na tuhuma za kushawishi wanakijiji wenzao kuvamia maeneo ya Shule ya Kilasara na kusababisha hasara kubwa kwa shule hiyo.
Kufuatia kukamatwa kwa watuhumiwa hao, wanakijiji waliamua kuaandamana hadi katika kituo cha polisi ili kuwatoa wenzao hali ilisababisha jeshi hilo kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya, jambo ambalo lilishindikana kutokana na wingi wa watu walikuwa wanaandamana.
Inadaiwa kuwa wananchi hao walijikusanya na walianza kuandamana kuanzia majira ya saa 7 usiku kuelekea kituo cha polisi ili kuwatoa wenzao walikuwa wanashikiliwa.
Wananchi wanaoshikiliwa na jeshi hilo ni John Sokoine, Abeli Solomoni, Christopher Solomon na aliyetambuliwa kwa jina moja tu la Julius. Wote walikamatwa usiku wa kuamkia jana.
Mnamo Juni 11, mwaka huu majira ya mchana wananchi wa kijiji hicho walivamia eneo lenye ukubwa wa hekta mbili na kufyeka mazao mbalimbali yaliyokuwa shambani hapo kwa madai kuwa wamiliki wa shule hiyo wamechukua eneo hilo kinyume cha taratibu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu, Kanda ya Afrika, Padri Jerome Okama, aliushutumu uongozi wa kijiji hicho kwa kuvifumbia macho vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi wakati wakitambua kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 8.9 linamilikiwa na shirika hilo kihalali.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Robert Boaz, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu kutoka wilayani humo jana jioni, alisema askari hao walipata ajali hiyo majira ya saa 6.45 mchana katika kijiji cha Kilingi nje kidogo ya mji wa Sanya Juu.
Alisema askari hao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na wengine wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu ya Kibong'oto ilioyopo wilayani Siha na kwamba watano kati yao hali zao ni mbaya.
Alitaja gari la Polisi lililopinduka na kuua kuwa ni Toyota Land Cruiser lenye namba PT 2070 lililokuwa likiendeshwa na Sajenti Herman Dancan. Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kuacha njia na kupinduka.
Aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Mkuu wa FFU mkoani hapa, ASP Nonino, Renatus Misigalo, Alfonce Joseph, Koplo Elifuraha Lenare, Peter Albert, Bashiri Yusuph, George Mwakyusa na Gaspar Mwapunda.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Kibong'oto.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment