FUNGA: TIBA ASILI YA KUPAMBANA NA MARADHI



Mungu alipoamrisha watu tufunge alikuwa na maana kubwa, ingawa baadhi ya waumini wanafunga ili kutimiza nguzo ya dini na pengine wengine hufunga huku wakiona kama ni adhabu na wangependa mwezi umalizike haraka, lakini hata tafiti kadhaa za kisayansi zimegundua kwamba funga huimarisha afya kwa kutibu na kuzui baadhi ya magonjwa.
Kiasili, miongoni mwa tiba asilia zenye nguvu ya kupambana na kutibu maradhi mengi mwilini ni funga. Watu wengi hivi sasa wameshaanza kugundua siri ya funga ambayo huwa dawa ya haraka kwa magonjwa mepesi kama vile mafua, kichwa, wasiwasi, n.k ambayo kwa mfungaji huwa hayana nafasi.
Inaelezwa na wataalamu wa tiba asilia ya Yoga kuwa funga ndiyo njia rahisi ya kuondoa sumu mwilini iliyorundikana kwa muda mrefu kutokana na ulaji wa vyakula usio sahihi. Utashangaa wakati wa funga utakapogundua kuwa mwili unahitaji kiasi kidogo sana cha chakula kila siku, kwani utajikuta una afya njema na ulaji wako ni wa kiasi kidogo tofauti na siku zingine.
Dalili moja wapo ya mtu mwenye tatizo litokanalo na mwili kuwa na sumu nyingi mwilini kutokana na vyakula anavyokula, ni kukosa hamu ya kula (appetite). Katika hili hakuna dawa zaidi ya kukaa bila kula ili kupata hamu ya kula.
Kukosa hamu ya kula ni njia moja wapo inayotumiwa na mwili kutoa taarifa kwamba sehemu kadhaa za viungo vya mwili zimejaa sumu, hivyo mwili unalazimika kutumia njia zake za asili kuzuia kuendelea kuingia kwa sumu na badala yake kufanya jitihada za kuitoa sumu nje.
Kwa mantiki hiyo, funga inakubalika kabisa na ile ‘filosofia’ inayosababisha magonjwa. Ikiwa magonjwa yanasababishwa na kurundikana kwa sumu katika mfumo wa mwili, ambayo huingia kwa njia ya vyakula tunavyokula, inaingia akilini pia kutumia funga kuondoa mrundikano huo wa sumu mwilini.

JE, MAZOEZI YANARUHUSIWA WAKATI WA FUNGA?
Kuna dhana kwamba mtu anayefunga hatakiwi kujishughulisha, badala yake anatakiwa kupumzika. Dhana hii siyo kweli na ni kosa kubwa kuacha kujishughulisha au kufanya mazoezi wakati wa funga.
Hakuna sababu yoyote ya msingi mtu asijishughulishe na kazi zake za kila siku kama kawaida, muhimu ni kuzingatia uwezo wako wa kufanya shughuli au mazoezi hayo bila mwili kuishiwa nguvu kabisa.

AINA ZA FUNGA
Kuna aina kadhaa za funga ambazo mtu anaweza kuzitumia kwa lengo fulani. Funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni funga ya ibada, ambapo mfungaji anapata thawabu kwa Muumba wake lakini pia anapata faida za kiafya za ujumla zinazotokana na funga.
Aina hii ya funga inajulikana pia kama DRY FAST, kwa maana mtu hatakiwi kula wala kunywa kitu chochote kuanzia alfajiri hadi magharibi jua linapozama, kwa muda wa siku 30 au 29. Mfungaji wa funga aina hii, licha ya kuwa ni ibada, anapata pia faida zote za kiafya tulizozieleza hapo juu.

0 comments:

Post a Comment