Polisi Asimulia Wanajeshi Walivyouawa Darfur

Askari wa JWTZ walionusurika na kifo wakiwa hospitalini kwa matibabu
Miili ya askari wa JWTZ waliofariki ikipewa heshima za mwisho za kijeshi kabla ya kusafirishwa kwenda Tanzania kwa mazishi.
Miili ya askari wa JWTZ waliouwawa na waasi ikipakiwa kwenye gari tayari kwa kusafirishwa kwenda Tanzania kwa mazishi. (Picha zote na Albert González, UNAMID)
WAKATI Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), likiwa bado halijatangaza rasmi majina ya wapiganaji wake waliofariki huko Sudan, askari polisi aliyeko huko ameeleza chanzo na mazingira ya tukio hilo. Wapiganaji saba na wengine 14 walijeruhiwa Jumamosi iliyopita.
Gazeti hili limepata majina ya askari hao waliofariki kutoka vyanzo tofauti lakini limeshindwa kuwataja leo kwa kuwa JWTZ kupitia kwa msemaji wake, Kanali Kapambala Mgawe limesisitiza kuwa haliwezi kutangaza majina hayo hadi litakapowasiliana na jamaa za askari waliofariki.
Tukio lilivyotokea
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, askari polisi huyo anayefanya kazi katika Mji wa Nyala uliopo Darfur, alisema mauaji hayo yalitokea wakati askari hao walipokuwa wakifuatilia magari yao yaliyokuwa yameporwa na kundi mojawapo la waasi.

Usalama katika Mji wa Nyala ambao ndiyo mkubwa zaidi katika eneo la Darfur, umekuwa mdogo katika siku za hivi karibuni. “Wale wanajeshi walikuwa doria ya kawaida, ila kama wiki moja iliyopita waasi walivamia tena doria ya wanajeshi wetu na kupora magari manne bila kuua mtu.
“Siku ya mauaji hayo wanajeshi wetu wakiwa tena katika doria waliyaona yale magari yaliyoporwa kwa mbali yamepaki, waliyafuatilia, walipokaribia kumbe ulikuwa mtego, wakashambuliwa,” alisema askari huyo na kuongeza: “Mauaji hayo yametokea takriban kilometa 70 kutoka katika kambi niliyopo mimi, lakini wote tupo eneo la kusini na hiyo kambi ya Korabeche inaongozwa na jeshi letu.”
Tofauti na chanzo chetu cha habari huko Darfur, Kanali Mgawe alisema wanajeshi hao walishambuliwa walipokuwa kwenye msafara wa kusindikiza walinzi wa amani.
Makundi yanayopambana
Askari huyo aliyeko Darfur alisema: “Makundi yanayopambana huku yapo mengi ila makubwa yapo kama matano. Kuna moja linaitwa Jeshi la Ukombozi la Watu wa Sudan (SPLA), ambalo limegawanyika katika makundi mawili pia kuna mengine kama JEM, Janjaweed na mengineyo.”

Akizungumzia mshtuko walioupata baada ya mauaji hayo, askari huyo alisema wafanyakazi wote wanaohusika na ulinzi wa amani wamepatwa na ganzi… “Huku kwa kweli hali imekuwa chungu, tangu askari hao wauawe hali haitabiriki kabisa, tupo nje hapa (hospitali walimohifadhiwa), tunasubiri uhakika.”
“Hawa jamaa (waasi), wamesheheni silaha na wana vifaa vya kisasa kiasi kwamba hata ndugu zetu walizidiwa kutokana na wenzao kuwa na silaha nzito, nikija Tanzania nitakuonyesha picha za mapambano yao,” alisema.
Akizungumzia kazi ambazo polisi wanazifanya huko, alisema hawaruhusiwi kushika silaha, bali kuwashirikisha wananchi katika masuala ya amani.
“Sisi majukumu yetu ni kuungana na jamii na kuwafundisha masuala mbalimbali, hivyo sisi tunawasiliana moja kwa moja na wananchi waliopoteza makazi kisha tunaandaa taarifa. Haturuhusiwi kushika silaha, wanajeshi wao wanatulinda na kusimamia usalama na kutusindikiza wakati wa doria,” alisema.
“Huku hali ya usalama haitabiriki. Mpaka sokoni tunakwenda chini ya ulinzi.”
Kauli ya JWTZ
Akizungumza kwa simu jana, Kanali Mgawe alikanusha uvumi wa majina yaliyosambaa mitandaoni huku akisema kwa utaratibu uliopo, jeshi haliwezi kutangaza majina hayo hadi ndugu watakapotaarifiwa. “Hayo majina yanayotajwa kwenye mitandao ni ya uongo. Kwa sasa mimi sijaletewa majina na utaratibu uliopo ni hadi ‘next of kin’ (ndugu) wao wajulishwe kwanza,” alidai Kanali Mgawe.

Hata hivyo, alisema Tanzania imewasilisha maombi ya kubadilisha kanuni za kulinda amani ikitaka kuruhusiwa kujihami kwa silaha za moto pale wanajeshi wake wanaposhambuliwa kwa kutumia kanuni namba saba ya Sheria za Majeshi ya Kulinda Amani.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz

0 comments:

Post a Comment